Home Vipindi Kundi la sekta mbalimbali la kushughulikia kesi za kimazingira lazinduliwa

Kundi la sekta mbalimbali la kushughulikia kesi za kimazingira lazinduliwa

0
Jaji Judy Omange wa mahakama ya mazingira
kra

Jaji Mkuu Martha Koome amezindua kundi la maafisa wa sekta mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa haki katika maswala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi katika kaunti ya Nairobi.

Kundi hilo litatoa kipaumbele kwa maswala hayo ya kimazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mkakati wa sekta mbali mbali.

kra

Jaji mkuu alisema idara ya mahakama imejitolea kushughulikia changamoto za kimazingira hasa mabadiliko ya tabianchi kwa kuhusisha kanuni za haki ya kimazingira.

“Hili litahusisha kujumuisha utunzaji wa mazingira kwenye shughuli, michakato na maamuzi yakiwemo matendo ya kiusimamizi na kimahakama.” Alisema jaji mkuu.

Koome alihimiza wanachama wa kundi hilo kuangazia kubuni utamaduni wa kikazi wa kushauriana na kushirikiana na mashirika mengine, na kuunda mfumo thabiti kati ya wadau ili kuharakisha utoaji huduma hasa za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Alipongeza kundi hilo kwa kujumuisha mfumo mbadala wa kupata haki katika kusuluhisha mizozo iliyosajiliwa kwenye kitengo hicho. Alikariri kwamba mfumo huo mbadala wa haki almaarufu AJS umebainika kuwa muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa haki.

Kulingana naye mfumo huo wa AJS unawapa watu wa jamii fursa ya kufahamu visababishi vya mizozo na kushirikiana kuviondoa na hatimaye kuhimiza marudiano na kuishi pamoja kwa amani.