Kampuni ya usafiri wa ndege ya Kenya Airways – KQ imetoa taarifa ya kuomba radhi wateja wake ambao safari zao zimecheleweshwa au kuvurugwa kwa njia moja au nyingine.
Kupitia taarifa jana jioni, usimamizi wa KQ ulielezea kwamba tatizo hilo linatokana na kuegeshwa kwa ndege zao mbili aina ya Boeing 787 Dreamliners.
Ndege hizo zina hitilafu kwenye injini zao na vifaa vya kuzikarabati vimecheleweshwa. Hilo limesababisha pia kukosekana kwa wahudumu wa ndege kwa baadhi ya safari.
Kampuni hiyo imeahidi kutatua matatizo hayo haraka iwezekanavyo na kurejelea safari zake kama kawaida, ikisisitiza kwamba usalama wa abiria na wahudumu wa ndege ni muhimu ndiposa wanajitahidi kurekebisha hali.
Taarifa hiyo ilielezea kwamba mtandao huenda ukawa sawa kufikia kesho Jumanne Mei 21, 2024 baada ya kupokea na kuwekea ndege hizo vifaa vinavyohitajika.