Mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei, ametoa changamoto kwa wadau katika sekta ya habari, mawasiliano na uchumi dijitali kuharakisha mabadiliko ya kidijitali.
Kulingana na Koskei, mabadiliko hayo ni nguzo muhimu katika kuafikia mpango wa serikali wa kukabiliana na ukosefu wa ajira humu nchini.
Aliongea hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa uwekaji mtandao wa internet katika kaunti ya Machakos, ambako alisifu hatua ya utoaji huduma za serikali kwa njia ya mtandao huo
Koskei ambaye aliandamana na waziri wa habari,mawasiliano na uchumi dijitali Eliud Owalo, alisema hatua hiyo itaboresha utoaji huduma na kuepusha mianya ya kupotezwa kwa mapato.
Aidha alionya kuhusu ongezeko la visa vya uraibu wa pombe miongoni mwa vijana ambao alisema unatishia udhabiti wa taifa hili.
Alisisitiza msimamo wa Rais William Ruto kuhusiana na ufisadi, huku akionya kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale wanaohusika na ufisadi.