Home Habari Kuu Koskei awatimua wakurugenzi sita na maafisa 67 wa polisi

Koskei awatimua wakurugenzi sita na maafisa 67 wa polisi

0

Mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei, amewasimamisha kazi maafisa sita wakuu watendaji na maafisa 67 wa polisi kwa kuhusika na ufisadi na makosa ya ununuzi.

Kupitia kwa taarifa iliyotolewa na msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed, time ya maadili na vita dhidi ya ufisadi imewaandikia mawaziri kadhaa, ikitaka maafisa  waliojihusisha na ufisadi kutimuliwa.

“Hatua hiyo ya Koskei inafuatia mapendekezo ya tume ya maadili na vita dhidi ya ufisadi EACC, yaliyotaka maafisa hao ambao Kwa sasa wanachunguzwa kusimamishwa kazi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo

Kulingana na Koskei, tume ya EACC imemwandikia waziri wa maji, usafi na unyunyiziaji mashamba maji Zachariah Njeru, ikipendekeza kusimamishwa kazi kwa afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya maji ya Tanathi mhandisi Fredrick Mwamati.

Mwamati anachunguzwa kwa makosa ya ununuzi katika utoaji zabuni kwa ujenzi wa mradi wa usambazaji maji wa Leather Industrial Park.

EACC pia imemwandikia waziri wa leba na ulinzi wa kijamii Florence Bore kumsimamisha kazi Mkurugenzi mkuu wa halmashauri ya kitaifa ya mafunzo ya kiviwanda NITA, kwa makosa za ununuzi kwa usambazaji bidhaa za halmashauri hiyo.

Wakati huo huo tume hiyo imeiandikia bodi ya usimamizi wa makavazi ya kitaifa ikitaka kutimuliwa kwa kaimu Mkurugenzi mkuu wake  Stanvas Ong’alo, kwa ufujaji wa shilingi milioni 490 kupitia malipo haramu.

Katika barua nyingine tume hiyo imetaka kutimuliwa kwa Mkurugenzi wa makao Makuu ya Huduma Center Benjamin Kai Chilumo, kwa madai ya ufisadi alipohudumu kwa serikali ya kaunti ya Kilifi kama afisa mkuu wa fedha.

Wengine ambao tume hiyo imependekeza watimuliwe ni pamoja na Mkurugenzi mkuu wa Bomas of Kenya Peter Gitaa Koria kwa madai ya ufisadi, meneja mkuu wa kampuni ya KETRACO mhandisi  Anthony Wamukota kwa makosa ya ununuzi na mhasibu wa  KeRRA Esther Wanjiru Chege, kwa kumiliki utajiri usioweza kuelezewa.

EACC pia imemtaka Inspekta mkuu wa polisi Japhet Koome, kuwatimuwa maafisa 67 wa polisi kwa makosa ya ufisadi.