Home Michezo Korea Kusini yampiga kalamu Jurgen Klinsmann

Korea Kusini yampiga kalamu Jurgen Klinsmann

0

Kocha Jurgen Klinsmann amepigwa kalamu na Korea Kusini baada ya timu hiyo kushindwa katika nusu fainali ya Kombe la bara Asia.

Chuma cha Klinsmann kiliingia motoni wakati Korea Kusini ilipopoteza mabao 2 – 0 dhidi ya Jordan Februari 6 .

Klinsmann alijiunga na Korea Kusini Februari mwaka uliopita kwa mkataba ambao ungekamilika baada ya Kombe la Dunia mwaka wa 2026.

Shirikisho la Kandanda la Korea (KFA) lilichukua uamuzi huo baada ya kupokea ushauri kutoka kwa kamati ya timu ya taifa Alhamisi iliyopita.

“Tumefikia makubaliano kuwa Klinsmann hawezi kuongoza timu ya taifa tena kwa sababu mbalimbali na kwamba mabadiliko ya uongozi ni muhimu,” alisema mkurugenzi wa kiufundi wa KFA Hwangbo Kwan.

Baada ya Korea Kusini kushindwa kwenye nusu fainali hiyo, mashabiki na wanasiasa walighadhabishwa na kutaka Klinsmann atimuliwe mara moja.

Hata hivyo,Klinsmann alidokeza kuwa hakuwa na mpango wa kujiuzulu kufuatia kichapo hicho.

Korea Kusini walipigiwa upatu kushinda taji kwenye mashindano hayo lakini hawakuridhisha uwanjani kwa matarajio ya mashabiki.

Alphas Lagat
+ posts