Home Habari Kuu Koome azungumzia kauli za Rais Ruto, asisitiza uhuru wa mahakama

Koome azungumzia kauli za Rais Ruto, asisitiza uhuru wa mahakama

0
Jaji Mkuu Martha Koome
Jaji Mkuu Martha Koome

Jaji Mkuu Martha Koome amekashifu matamshi ya Rais William Ruto ya kupuuza maagizo ya mahakama akisema yanatishia uhuru wa idara hiyo.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari jana Jumatano jioni, Koome, kupitia Tume ya Huduma za Mahakama, JSC japo hakutaja jina la Rais, alisema vitisho dhidi ya majaiji na mahakama kwa jumla ni kinyume cha sheria na huenda vikaleta hali ya mapuuza ya sheria.

Kumekuwa na shutuma kali kutoka kwa makundi mbalimbali dhidi ya hotuba ya Rais Ruto katika sherehe za mwaka mpya, akiapa kupuuza maagizo ya mahakama ya kusitisha mipango yake ya maendeleo.

Chama cha Majaji na Mahakimu, kile cha Wanasheria Nchini, LSK na kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga ni miongoni mwa waliokashifu matamshi ya Rais.

Hata hivyo, Rais Ruto ameapa kuwa hataruhusu watu wachache kuitumia idara ya mahakama kuhujumu mipango ya serikali.

Ruto anasema baadhi ya majaji wafisadi wanashirikiana na watu hao kuhujumu mipango ya serikali ya Kenya Kwanza, akitaja mpango wa nyumba za gharama nafuu na ule wa afya kwa wote, ambapo kesi zimewasilishwa mahakamani kupinga utekelezaji wake.