Jaji Mkuu Chief Martha Koome ameitaka huduma ya kitaifa ya Polisi kurejesha walinzi wa Jaji Lawrence Mugambi mara moja.
Inadaiwa kuwa walinzi wa jaji huyo wa mahakama kuu walitolewa siku kadhaa baada yake kumhukumu kifungo cha miezi sita gerezani kaimu Inspekta Mkuu wa Polisi Gilbert Masengeli.
Akizungumza kwenye kikao cha Wanahabari Jumatatu,Koome ambaye pia ni mwenyekiti wa tume ya wafanyikazi wa mahakama, amelaani kitendo hicho akisisitiza umuhimu wa idara ya mahakama kufanya kazi bila mapendeleo wala kushurutishwa.
Koome amesema hatua hiyo inahujumu uhuru wa mahakama na kuhatarisha taifa kuwa na hulka ya kutojali sheria.
Jaji Mugambi alimhukumu Masengeli kifungo cha miezi sita gerezani baada yake kupuuza mahakama mara tatu, alipoitwa kujibu maswali kuhusu watu waliotoweka wakati wa maandamano ya kupinga serikali.
Mugambi alipokonywa walinzi wake mwishoni mwa juma lililopita.