Jeshi la Kenya KDF limetangaza kwamba kongamano la mwaka huu la shirika la watafiti wa maeneo ya mipakani yaani African Borderlands Research Network litaandaliwa kesho jijini Nairobi.
Kulingana na KDF mkutano huo wa kila mwaka utaandaliwa kwenye taasisi ya usaidizi wa kibinadamu na amani katika eneo la Embakasi kuanzia saa mbili asubuhi.
Lengo la kongamano hilo ni kujadili majibu ya utafiti muhimu, kujadili taswira sawia katika maeneo mbali mbali barani Afrika na kupata maoni ya wasomi kuhusu jinsi ya kutumia sera zilizopendekezwa kupitia mipango inayowezekana na itakayoleta athari faafu katika maeneo ya mipakani.
Waziri aliye na mamlaka makuu ambaye pia ni waziri wa masuala ya kigeni Musalia Mudavadi ataongoza ufunguzi wa kongamano hilo.
Shirika hilo linalojumuisha maafisa kutoka vitengo mbali mbali lilibuniwa mwaka 2007 na kufikia sasa lina wanachama wapatao 300 wengi wao wakiwa bara Uropa, Afrika na Amerika Kaskazini.
Wasomi hao wanajihusisha na masuala yote ya mipaka ya kimataifa na matukio ya mipakani. Huwa wanaangazia sio tu maeneo ya mipakani kama nafasi tupu bali pia kama maeneo ambapo jamii zinatagusana na jinsi usafiri wa watu na usafirishaji wa bidhaa unafanyika.
Shirika hilo linadhamiria kubuni mtazamo mmoja kuhusu maeneo ya mipakani barani Afrika ambao utajuzwa wasomi, waunda sera pamoja na wanafunzi.
Hatua hiyo itachangia uelewa wa ndani zaidi kuhusu mataifa na maeneo yao ya mipakani kijumla ili kusaidia katika uundaji sera barani Uropa, Afrika na kwingine.