Nadhari ya dunia inaelekezwa kwa jiji kuu la Kenya, Nairobi katika kipindi cha siku tatu zijazo.
Hii ni kwa sababu kuanzia hii leo Jumatatu, jiji hilo litakuwa mwenyeji wa Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi litakaloandaliwa katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta, KICC.
Rais William Ruto anatarajiwa kufungua rasmi kongamano hilo la kihisitoria litakalohudhuriwa na angalau wakuu wa nchi na serikali 20.
Kwa jumla, wajumbe wapatao 30,000 kutoka kote duniani wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo na wengi wao walitua nchini kuanzia jana Jumapili.
Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi linatarajiwa kuweka ajenda ya namna bara la Afrika litashirikiana na jumuiya ya kimataifa kuhusiana na masuala ya utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi siku zijazo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Dkt. Alfred Mutua amelitaja kongamano hilo kuwa fursa muhimu ya Afrika kuungana juu ya masuala yote yanayohusiana na mabadiliko ya tabia nchi.
Dkt. Mutua anasema kwa mara ya kwanza, Afrika itazungumza kwa sauti moja kuhusiana na masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na mipango ya ufadhili kwa kusudi la kukabiliana na athari zake.
Ili kufuatia matukio yote yanayofungamana na kongamano hilo, usikose kutembelea tovuti hii na ile ya Kiingereza ambayo ni www.kbc.co.ke kwa habari za hivi punde zaidi na pia kutazama runinga ya KBC Channel One na kusikiliza idhaa zetu za redio kwa uchambuzi wa kina kuhusiana na yote yatakayojiri.