Chama cha Madaktari, wataalam wa dawa na meno, KMPDU kimesema kuwa zaidi ya madaktari 4,000 hapa nchini hawana ajira, ikizingatiwa upungufu wa madaktari unaoshuhudiwa katika vituo vya afya vya umma.
Huku kikiandaa maandamano ya amani nje ya jumba la Afya Jijini Nairobi, chama hicho kilisema kinasikitishwa na ukosefu wa dawa za kutosha na wahudumu wa kutosha wa afya katika hospitali za umma.
“Madaktari waliofuzu hivi maajuzi hawajaajiriwa. Zaidi ya madaktari 4,000 hapa nchini hawana ajira, licha ya kuwa na upungufu wa madaktari katika hospitali za hapa nchini,” KMPDU ilisema kupitia mtandao wake wa twitter.
Aidha akiwahutubia madaktari hao nje ya jumba la afya, Waziri wa Afya Susan Nakhumicha aliwahimiza madaktari hao kuhusika katika kutafuta suluhu kwa changamoto zinazokumba sekta ya afya, katika juhudi za kuimarisha huduma za afya hapa nchini.
Waziri Nakhumicha alikiri kwamba wizara hiyo imepokea rufaa kutoka kwa chama cha KMPDU huku akisema kwamba ipo haja ya kuimarishwa kwa huduma za afya nchini.
Nakhumicha alitoa hakikisho kwamba atashauriana na wadau wengine wakuu husika, likiwemo bunge la taifa na baraza la magavana kabla ya kuwasilisha suluhu mwafaka kwa chama hicho.