Chama cha madaktari, wataalam wa dawa na madakari wa meno, kinasisitiza kwamba kitaanza mgomo Jumatano usiku wa manane, kufuatia kusambaratika kwa mazungumzo kati yao na serikali.
Katibu mkuu wa chama hicho Dkt. Davji Atellah amesema mikutano miwili na wizara ya afya haikuafikia chochote huku wakiilaumu serikali kwa kuosa kutimiza baadhi ya matakwa yao yasiyohitaji matumizi yoyote ya fedha.
Chama hicho kimesema serikali ilikosa kuonyesha ari na azma ya kushughulikia maswala yaliyoibuliwa na kuwalazimisha kususia kazi.
Matakwa mengine ni pamoja na kupandishwa vyeo, bima ya matibabu, malipo ya karo ya kuendeleza masomo, likizo ya masomo na kutendewa haki kwa katibu mkuu wa chama hicho Dkt.Davji Atellah ambaye alijeruhiwa wakati wa maandamano ya amani yaliyofanyika tarehe 29 mwezi Februari mwaka huu.