Home Habari Kuu Kituo cha kuratibu mipango ya kukabiliana na mafuriko chabuniwa

Kituo cha kuratibu mipango ya kukabiliana na mafuriko chabuniwa

0

Wizara ya mambo ya ndani imetangaza kwamba kituo cha kuratibu mipango na mawasiliano kuhusu kukabiliana na athari za mvua kubwa inayonyesha nchini hasa mafuriko kimebuniwa.

Kituo hicho kiko katika jengo la Nyayo jijini Nairobi na kimejukumiwa kusajili na kutoa ripoti zote kuhusu matukio ya mafuriko.

Kundi la wawakilishi wa wizara 11 na mashirika husika watahudumu katika kituo hicho kupitia mpango wa serikali yote na watatoa tahadhari kuhusu mafuriko, kuratibu mipango ya kujitayarisha kwa mafuriko, kuhakikisha usalama wa wakazi na kushughulikia dharura zozote.

Wizara hizo ni pamoja na ile ya ulinzi, ya mambo ya ndani, ya barabara, ya afya, ya elimu, ya maji, ya ardhi, ya nyumba, ya kilimo, ya kawi, ya masuala ya afrika mashariki na maeneo kame na ile ya leba.

Mashirika ya ulinzi ambayo ni jeshi la KDF, huduma ya taifa ya polisi, huduma ya wanyamapori, huduma ya ulinzi wa fuo na shirika la huduma ya vijana kwa taifa NYS nayo yameshirikishwa.

Katibu wa usalama wa ndani Daktari Raymond Omollo, aliandaa kikao na wanahabari kuelezea kuhusu mipango ya kukabiliana na athari za mafuriko leo alasiri.

Alielezea kwamba baraza la magavana na shirika la msalaba mwekundu wamejulishwa na kuombwa kusaidia katika kufadhili mipango inayotekelezwa.

“Kuokoa maisha na kupunguza athari za mvua ya El Nino kupitia tahadhari za mapema na ufuatiliaji unasalia kuwa jukumu muhimu kwa serikali.” alisema Omollo.

Kundi hilo limejukumiwa pia kukusanya mapato ya kufadhili mipango ya kukabiliana na athari za mafuriko.

Katika mawasiliano yake leo, Omollo alifichua kwamba kaunti 4 za Tana River, Garissa, Wajir na Mandera zimetambuliwa kama zilizoathirika zaidi na mafuriko ambapo watu 120 wameaga dunia.

Kaunti 10 ambazo ni Isiolo, Samburu, Kwale, Homabay, Makueni, Tharaka Nithi, Lamu, Taita Taveta, Meru na Kisumu zimeorodheshwa kama zilizo katika tahadhari kubwa.

Familia elfu 89, zimepoteza makazi na kwa sasa zimepatiwa hifadhi katika kambi 112 katika kaunti zilizoathirika.

Misaada ya chakula, maji na vifaa vingine imewasilishwa katika kaunti kadhaa na mipango hiyo bado inaendelea.

Website | + posts