Huku mazungumzo kati ya Kenya Kwanza na muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ukitarajiwa kung’oa nanga siku ya Jumatano katika ukumbi wa Bomas, upande wa Azimio umemteua aliyekuwa mbunge wa Ndaragua Jeremiah Kioni kuongoza kundi la kiufundi na kisheria la Muungano huo.
Muungano huo wa Azimio pia umemteua kiongozi wa wachache bungeni Opiyo Wandayi kuwa naibu mwenyekiti na msemaji wa ujumbe wa Azimio katika mazungumzo hayo.
Kiongozi wa Azimio Raila Odinga, alisema hatua hiyo inalenga kupiga jeki ujumbe wa muungano huo katika mazungumzo hayo aliyoyataja kuwa muhimu sana katika kutatua changamoto zinazoghubika taifa hili.
Akizungumza siku ya Jumanne baada ya kuandaa mkutano na viongozi wa Muungano huo Jijini Nairobi, Raila aliwaagiza wajumbe wa Azimio na wenzao wa Kenya Kwanza kushiriki mazungumzo hayo kwa uwazi, heshima na kukamilisha mazungumzo bila kuchukua muda mrefu kwa manufaa ya wakenya.
“Tumejitolea kushiriki meza ya mazungumzo kwa nia njema, kwa lengo la kutatua changamoto zinazokabili taifa hili. Tunatoa wito kwa mazungumzo yatakayozingatia uwazi, heshima na maadili,” alisema Raila Odinga.
Maswala ambayo upande wa Azimio unataka yajadiliwe ni pamoja na gharama ya juu ya maisha, kubuniwa kwa tume huru ya uchaguzi na mipaka, mikakati ya kuzuia kuingiliwa kwa vyama vya kisiasa na maswala mengine ya kikatiba.
Wajumbe wa Azimio katika mazungumzo hayo ni pamoja na Kalonzo Musyoka, Opiyo Wandayi, Eugene Wamalwa, Okongó Omogeni na Amina Mnyazi.