Home Kimataifa King’ori Mwangi, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi wa zamani afariki

King’ori Mwangi, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi wa zamani afariki

0
kra

Aliyekuwa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi King’ori Mwangi amefariki. Tangazo la kifo chake limetolewa leo Jumapili, Februari 11, 2024 na familia yake.

Mwangi alikata roho akiendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Nairobi.

kra

Kulingana na tangazo hilo, Mwangi alikuwa amefanyiwa upasuaji hospitalini humo na baadaye afya yake ikazorota na kusababisha kifo chake.

Familia hiyo imeahidi pia kujuza umma kuhusu mipango ya mazishi.

King’ori Mwangi alihudumu kama Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi hadi mwaka 2018 ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Japhet Koome. Baada ya hapo, alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje hadi alipostaafu.

Aliwahi kuhudumu kama mkuu wa mipango katika makao makuu ya huduma ya taifa ya polisi, kama msemaji wa polisi, kama mkurugenzi wa taasisi ya kutoa mafunzo kwa maafisa wa polisi huko Kiganjo na msaidizi mkuu.

King’ori alikuwa ameweka mambo ya familia yake kuwa siri isipokuwa visa vichache ambavyo vilifahamika kama kifo cha mke wake Mercy Wangari mwaka 2019.

Mwaka 2021, aligonga vichwa vya habari baada ya gari alilokuwa akiendesha kugonga watu wawili huko Lang’ata, na ikabainika kwamba alikuwa akikimbiza mwanamke mjamzito hospitalini.

Agosti mwaka huo, alizungumziwa tena baada ya makazi yake kuvamiwa na wezi waliowashika mateka wafanyakazi wake wa nyumbani ambao walitekeleza wizi huo kwa saa nane na kuondoka na bidhaa za thamani ya juu na bunduki yake.

Website | + posts