Waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki, amezindua kambi ya kitengo cha maafisa wa polisi wa kukabiliana na wezi wa mifugo katika eneo la Mulango kaunti ya Isiolo, huku serikali ikiahidi kukabiliana vilivyo na wizi wa mifugo katika eneo hilo.
Huku akizindua kambi hiyo, waziri huyo aliwaonya majangili katika eneo hilo kwamba watakabiliwa vilivyo na serikali iwapo hawatabadili mienendo yao.
Alidokeza kuwa maafisa wa polisi wamepewa maagizo ya kutumia silaha zao kulinda maisha na mali, kwa mujibu wa sheria za Kenya.
Aidha Prof Kindiki alisema serikali imewapoteza maafisa kadhaa wa polisi mikononi mwa wahalifu, hali aliyosema haitavumiliwa tena na serikali.
Aliongeza kuwa serikali itaanzisha kambi mbili za usalama katika eneo la Yamicha na Biliqo, katika juhudi za kukabiliana na ujangili katika eneo hilo.
Viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na Gavana wa Isiolo Abdi Ibrahim Guyo, walipongeza hatua hiyo ya serikali ya kupeleka kikosi hicho cha polisi katika eneo la Mulango, akiitaja kuwa hatua muhimu ya kukabiliana na ujangili miongoni mwa jamii za wafugaji.
Gavana huyo alitoa wito kwa serikali ya kitaifa kuhakikisha mifugo walioibwa wanatafutwa na kurejeshewa wenyewe.