Ili kuafikiwa kwa amani ya kudumu na udhabiti hapa nchini, kunahitaji msimamo mkali katika kukabiliana na vitisho vya usalama wa taifa hili, amesema waziri wa usalama wa taifa Prof. kithure Kindiki.
Akizungumza mjini Mombasa Jumanne, waziri Kindiki alisema serikali inapiga jeki vita dhidi ya utovu wa usalama, kwa boresha vifaa vinavyotumiwa na maafisa wa polisi.
Waziri huyo alidokeza kuwa serikali itatumia kitita cha shilingi bilioni 37 katika mpango wa kuboresha vifaa vya polisi katika kipindi cha miaka mitano.
“Ili kushinda vita dhidi ya ugaidi, ujangili na magenge ya wahalifu, serikali inatekeleza mpango wa shilingi bilioni tano wa kuimarisha vifaa vya maafisa wa polisi,” alisema waziri Kindiki.
Aliyasema hayo baada ya kupokea na kuzindua magari mapya ya kuwasafirisha maafisa wa polisi.
Kindiki alisema kupokelewa kwa vifaa vya kisasa vya maafisa wa polisi, ni hatua kubwa katika kuhakikisha taifa hili ni salama , na kukabiliwa vilivyo kwa magenge ya majangili .