Home Habari Kuu Kindiki: Serikali haitawavumilia wanaofadhili na kuchochea ghasia

Kindiki: Serikali haitawavumilia wanaofadhili na kuchochea ghasia

Waziri huyo aliwalaumu baadhi ya wanasiasa kwa kufadhili na kuchochea utovu wa usalama katika eneo hilo.

0
Waziri wa Usalama Kithure Kindiki aongoza mkutano wa usalama kaunti ya Nyamira.

Waziri wa Usalama wa Kitaifa Kithure kindiki amewaonya vikali wanaochochea ghasia katika kaunti ya Nyamira, akisema wanadumaza maendeleo na wanasababisha kupotea kwa maisha.

Waziri huyo aliwalaumu baadhi ya wanasiasa kwa kufadhili na kuchochea utovu wa usalama katika eneo hilo.

Kindiki alisema uhasama kati ya kiranja wa wengi katika bunge la taifa Sylvanus Osoro na Gavana wa kaunti ya Kisii Simba Arati unazidisha utovu wa usalama katika eneo hilo.

Viongozi hao wawili wamekuwa wakirushiana cheche za maneo, huku kila mmoja akimtishia mwenzake na kusababisha kutekelezwa kwa visa vya uhalifu.

Hivi majuzi, kundi la vijana lilimzomea Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu wakati wa hafla moja ya mazishi.

Waaidha, Waziri Kindiki alisema wanaochochea vurugu bila kujali miegemeo yao ya kisiasa hawatavumiliwa.

Aliyasema hayo leo Ijumaa alipoongoza mkutano wa kiusalama katika kaunti ya Nyamira.