Waziri wa usalama wa kitaifa Prof. Kithure Kindiki, amesema serikali itazindua mchakato wa kitaifa Jumatano wiki ijayo, kuhakikisha Pasipoti zilizoko katika afisi za uhamiaji zinachukuliwa.
Hatua hiyo inajiri baada ya waziri huyo kudokeza kuwa kuna idadi kubwa ya pasipoti ambazo hazijachukuliwa katika afisi zote za uhamiaji kote nchini.
Akizungumza alipofanya ziara ya ghafla katika afisi ya uhamiaji ya Embu siku ya Jumanne, waziri Kindiki alisema pasipoti 30,000 hazijachukuliwa katika afisi ya Nairobi, huku pasipoti 6,000 zikikosa kuchukuliwa katika afisi ya uhamiaji ya Embu.
Alisema serikali itawashurutisha waliotuma maombi ya pasipoti kuzichukua katika muda utakaotangazwa Jumatano ijayo.
“Huwezi shinikiza maafisa wa uhamiaji wakupatie pasipoti, lakini baada ya kuchapishwa kwa pasipoti hiyo, huji kuchukua,”alifoka Kindiki.
Wakati huo huo, waziri alisema serikali itaongeza idadi ya wafanyikazi katika afisi ya uhamiaji ya Embu kutoka idadi ya sasa ya wafanyikazi 20 hadi 30, ili kuimarisha utoaji huduma.