Home Habari Kuu Kindiki: Kenya haitagharimika kutuma polisi Haiti

Kindiki: Kenya haitagharimika kutuma polisi Haiti

0

Waziri wa Mambo ya Ndani Prof. Kithure Kindiki ameelezea kwamba serikali ya Kenya haitagharimika kwa vyovyote kwenye mpango wa kutuma maafisa wa polisi nchini Haiti.

Kwenye taarifa kupitia akaunti iliyothibitishwa ya Facebook, Prof. Kindiki alisema mpango mzima unafadhiliwa na Umoja wa Mataifa kupitia michango ya nchi wanachama.

Alisisitiza kwamba mpango huo hautaathiri kujitolea kwa serikali kutekeleza jukumu lake la kulinda maisha na mali ya Wakenya.

“Harakati za kutafuta na kukamata wezi, magaidi na majangili waliojihami zitaendelea serikali inaposawazisha majukumu ya kitaifa na kimataifa,” alisema Prof. Kindiki.

Waziri huyo ambaye alihudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa la Kithurine Methodist katika eneo bunge la Imenti ya Kati, alisema ni heshima kubwa kwa Kenya kuchaguliwa kuongoza kikosi cha polisi nchini Haiti na ana imani kwamba kitafanikiwa.

“Tutafanikiwa nchini Haiti jinsi tulivyofanikiwa katika mipango ya awali ya kudumisha amani katika nchi kama vile Chile, Jamaica, Grenada, Paraguay, Burundi, Chad, Nigeria na Mauritius.”

Waziri Kindiki alionya dhidi ya maandalizi ya mikutano ya kukashifu au kuchochea wananchi dhidi ya viongozi fulani akirejelea joto la kisiasa linalodhihirika katika kaunti ya Meru.

Aidha alitangaza kurejeshwa kwa mifugo walioibwa akisema wezi katika mpaka kati ya kaunti za Meru na Isiolo watakabiliwa vilivyo.