Home Kimataifa Kimbunga Hidaya chatua kusini ya Tanzania

Kimbunga Hidaya chatua kusini ya Tanzania

kimbunga Hidaya.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga Hidaya kilichopo karibu na maeneo ya pwani ya Tanzania.

Taarifa yake imesema hadi kufikia saa 9 usiku wa kuamkia leo Jumamosi, Kimbunga hicho kilikuwa katika eneo la bahari takriban kilomita 125 kutoka pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi), kilomita 93 kutoka pwani ya Mafia na kilomita 128 kutoka pwani ya Dar es salaam na kasi ya upepo unaofika kilomita 120 kwa saa.

Tangu usiku wa kuamkia leo, matukio ya upepo mkali na mvua kubwa zinazosababishwa na uwepo wa kimbunga yameendelea kujitokeza ambapo hadi kufika saa 3 asubuhi, kituo cha hali ya hewa cha Kilwa Masoko (Lindi) kimeripoti mvua ya jumla ya kiasi cha milimita 111.3 kwa kipindi cha saa 6 zilizopita.

Kiwango hiki cha mvua ni kikubwa sana ukizingatia kuwa wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko ni milimita 96.6 tu. Hivyo kiasi cha mvua kilichonyesha ndani ya saa 24 katika kituo cha Kilwa Masoko ni takribani asilimia 115 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko.

Viwango vya mvua vilivyopimwa katika vituo vingine katika kipindi hicho ni milimita 90.7 kwa Mtwara na milimita 85.3 katika kituo cha hali ya hewa Naliendele (Mtwara). Kiwango cha mvua cha milimita 90.7 kilichonyesha Mtwara ndani ya saa 24 ni takribani asilimia 168 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa Mtwara (milimita 54).

Vipindi vya mvua kubwa bado vinaendelea katika maeneo hayo ya ukanda wa pwani ya kusini. Kwa upande mwingine, katika vituo vya hali ya hewa vya Mtwara, Kilwa, Zanzibar, Tanga na Dar es Salaam upepo mkali unaozidi kilomita 50 kwa saa umeweza kupimwa katika nyakati tofauti kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi asubuhi ya leo.

Aidha, kimbunga kinatarajiwa kuendelea kusogea karibu zaidi na ukanda wa pwani ya Tanzania huku kikipungua nguvu taratibu kuelekea usiku wa kuamkia Jumapili tarehe 05 Mei 2024.

Kimbunga bado kinatarajiwa kuendelea kusababisha matukio ya vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa pwani hususan mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es salaam pamoja na kisiwa cha Unguja na maeneo ya jirani. Vilevile, matukio ya mawimbi makubwa baharini yanatarajiwa kuendelea kujitokeza katika ukanda wote wa mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi.

Wananchi wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wameshauriwa kuchukua tahadhari kubwa.