Kocha mkuu wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 Simon Jawichre, amekitaja kikosi cha wachezaji 28 kitakachoshiriki mashindano ya mwaka huu ya bara Afrika ya kuwania kombe la Barthes yatakayoandaliwa tarehe 20 hadi 28 mwezi huu mjini Harare, Zimbabwe.
Edmond Omondi atakiongoza kikosi hicho akiwa nahodha pamoja na Geylord Ngasi, Andycole Omollo, Iddo Kuta na Wycliffe Ogutu miongoni mwa wachezaji wengine. Michuano ya mwaka huu itashirikisha timu nne zikiongozwa na wenyeji Zimbabwe, Kenya, Namibia na Tunisia.
Timu hizo zitamenyana kwa siku tatu huku timu itakayomaliza ya kwanza ikishinda taji hiyo ya Barthes na kufuzu kuwakilisha Afrika katika mashindano ya Raga Duniani kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka ishirini kuanzia tarehe 2 hadi 7 mwezi Julai nchini Scotland.
Timu ya taifa itaondoka humu nchini Alhamisi hii kabla ya kushirki mchuano wao wa ufunguzi dhidi ya Namibia siku ya Jumamosi na kisha kumenyana na Tunisia Jumatano wiki ijayo kabla kuhitimisha ratiba dhidi ya wenyeji na mabingwa watetezi Zimbabwe tarehe 28 mwezi huu…