Shirika la Kutetea Haki za Binadamu nchini, KHRC limepinga ombi la Kenya la kutaka kujiunga na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, UNHRC kwa kipindi cha mwaka 2025-2027.
Kenya ilituma ombi hilo Septemba 27, 2024 na kuahidi kupigania na kulinda haki za binadamu za watu wote nchini.
Hata hivyo, KHRC na washirika wake wanadai ahadi ya Kenya inakinzana na hali halisi nchini.
Mashirika hayo yamemwandikia barua Rais wa UNHRC yakipinga ombi la Kenya.
“Tumeorodhesha sababu kadhaa, ikiwa ni pamoja na ukiukaji wa kimfumo wa haki za binadamu unaokaribiana na uhalifu dhidi ya binadamu,” inasema KHRC katika taarifa.
Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, UN zitakutana leo Jumatano jijini New York nchini Marekani kupigia kura ombi la Kenya.
Pingamizi hizo zinakuja wakati maafisa wa polisi nchini wameshutumiwa kwa jinsi walivyokandamiza waandamanaji wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z miezi minne iliyopita.
Aidha, mashirika hayo yanaituhumu serikali kwa visa vya utekaji nyara ambavyo vimeripotiwa nchini katika siku za hivi karibuni.