Mwanamuziki wa mtindo wa Hip Hop nchini Kenya Khaligraph Jones ametoa kibao kipya kwa jina “Bongo Favour” baada ya kuanzisha mzozo kati ya wanamuziki wa mtindo huo wa kufokafoka wa Kenya na Tanzania.
Siku chache zilizopita, Papa Jones alitumia akaunti yake ya mtandao wa Instragram kualika wanamuziki wa Hip Hop wa Tanzania kwenye shindano la kufokafoka naye.
Alisema anaamini anawazidi wote kwa weledi wa kufokafoka na akawapa muda wa saa 24 kumjibu la sivyo ajitangaze mwanamuziki bora wa rap nchini Tanzania.
Alisema yeye ndiye bora katika muziki wa rap nchini Kenya na Nigeria kwa sasa huku akitambua young Lunya pekee kutoka Tanzania.
Mwanamuziki huyo ambaye pia hujiita OG alijibiwa na wanamuziki wengi wa Tanzania akiwemo Harmonize ambaye hivi maajuzi ameshirikiana na Khali kwenye kibao kiitwacho “Kwame”.
Harmonize alimkumbusha Papa Jones kuhusu ushirikiano wao na kumsihi awe makini na asifananishe muziki wa rap wa Tanzania na Amapiano.
Mmiliki huyo wa kampuni ya muziki ya Konde alitaja wanamuziki kama Weusi na Professor Jay kuwa wakali wa Hip Hop Tanzania akiongeza kwamba kiwango cha Papa Jones ni cha Lunya na country boy lakini bado wanamshinda.
Rapa wa kike wa Tanzania Rosa Ree naye amemjibu Khaligraph kwa video ya kibao cha rap ambacho alirekodi ambacho Papa Jones alikitaja tu kuwa ‘jaribio zuri’.
Rosa alilazimika kujibu kwa maneno akisema hawamwogopi Khali na kwamba hata kama ana misuli kutokana na mazoezi makali akifika Tanzania watambeba yeye pamoja na ‘gym’.
Fido Vato, aliyekuwa mmoja wa wanachama wa kundi la muziki wa rap nchini Tanzanian Nako 2 Nako naye hakusaazwa katika kujibu Khaligraph akisema awali alikubali kutambua wanamuziki wa Tanzania lakini sasa anajifanya mkubwa kuwazidi.
“Arusha sio mbali na Kenya. Ni masaa mawili tu. Abiri basi, uje tumenyane ndondi na rap.” alisema Vato akiongeza kusema kwamba Khali ana mwili mkubwa na sauti ndogo kama ya mpenzi wake!
Khaligraph amewajibu rasmi kwa kutoa kibao hicho kiitwacho Bongo Favour tazama;