Kesi ya kubanduliwa mamlakani kwa Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza itasikilizwa na kikao cha bunge lote la Seneti.
Hii ni baada ya maseneta kupinga mjadala uliokuwa umewasilishwa na Seneta wa kaunti ya Kakamega Bonny Khalwale uliopendekeza suala hilo kusikilizwa na kamati teule.
Baada ya kupata fursa ya kuchangia mjadala huo maseneta kwa njia ya kupaaza sauti zao wakiongozwa na Spika wa bunge hilo Amazon Kingi waliupinga na hivyo kupendelea kikao cha bunge lote.
Khalwale ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge la Seneti alikuwa amependekeza maseneta Hillary Sigei, Abdul Hajji, Wahome Wamatinga, David Wafula, Gloria Orwoba, Karen Nyamu, Boy Issa Juma, Eddie Oketch, Shakila Abdalla, Beth Mundet na Beatrice Akinyi kuwa wanachama wa kamati teule ambayo ingesikiliza suala la kubanduliwa mamlakani kwa Gavana Mwangaza.
Akichangia mjadala huo, Seneta wa Narok Ledama Ole Kina alisema kwamba masuala yanayoibuliwa katika suala hilo ni mazito na iwapo uamuzi wake utakabidhiwa kamati, huenda uamuzi huo ukatiliwa shaka na umma.
Seneta wa Nandi Samson Cherargei kwa upande wake alitaka uchunguzi na uamuzi wa suala hilo zima ufanywe kwa njia ambayo wakenya wote wanaweza kufuatilia.
Alitania kwamba iwapo uamuzi huo utafanywa kwa faragha, kizazi cha Gen Z huenda kikasalimia maseneta.
Seneta Karen Nyamu kwa upande wake alitaka kamati teule ambayo angekuwa mwanachama ipatiwe fursa ya kusikiliza kesi hiyo maoni sawia na ya seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.