Home Kimataifa Kesi dhidi ya mbunge wa Tanzania Pauline Gekul yafutiliwa mbali

Kesi dhidi ya mbunge wa Tanzania Pauline Gekul yafutiliwa mbali

0

Kesi ya ukatili iliyowasilishwa katika mahakama ya wilaya ya Babati dhidi ya mbunge wa Babati Mjini nchini Tanzania Pauline Gekul imefutiliwa mbali.

Gekul alikuwa ameshtakiwa kwa kile kinachodaiwa kuwa kumnyanyasa mfanyakazi wake wa nyumbani kwa jina Hashim Ally.

Hakimu wa Mahakama hiyo ya Wilaya Babati Victor Kimario alielezea kwamba kesi hiyo iliyotajwa leo Disemba 27, 2023 imefutiliwa mbali baada ya mkurugenzi wa mashtaka kusema kwamba hangependa kuendelea nayo.

Alisema pia kwamba hakuna wakili wa upande wa serikali alifika mahakamani wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo.

Hashim aliwasilisha kesi hiyo mahakamani kupitia kwa wakili wake Peter Madeleka chini ya kifungu nambari 128 sehemy ya 2 na ya 4 cha Sheria ya Makosa ya Jinai.

Kulingana na wakili Madeleka sheria hiyo inaruhusu mtu binafsi kuwasilisha kesi ya jinai dhidi ya mwingine bila kuhusisha afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma.

Mbunge huyo alikuwa anakabiliwa na shtaka la kumshambulia Hashim na kumsababishia madhara mwilini.

Inadaiwa kwamba Gekul na watu wengine walimzuilia Hashim katia eneo la Babati huku wakimtishia kwa bastola kisha wakamvua nguo na kumlazimisha akalie chupa ambayo iliingia katika sehemu zake za siri.

Kisa hicho kinakisiwa kuwa sababu kuu ya Rais Samia Suluhu Hassan kutengua uteuzi wa Pauline Gekul kama naibu waziri wa masuala ya haki na sheria.

Website | + posts