Home Habari Kuu Kenya yaunga mkono ushirikiano na nchi nyingine katika vita dhidi ya mihadarati

Kenya yaunga mkono ushirikiano na nchi nyingine katika vita dhidi ya mihadarati

0
Beverlyne Opwora, Prof Muteti na Mohammed Buba Marwa

Kenya inaunga mkono wazo la ushirikiano na mataifa mengine katika kukabili ukuzaji na maandalizi ya mihadarati na madawa mengine ya kulevya.

Akizungumza jijini Abuja nchini Nigeria katika kongamano la 31 la wasimamizi wa mashirika ya kitaifa ya kupambana na mihadarati, Beverly Opwora anayeongoza ujumbe wa Kenya katika kongamano hilo alisema kwamba Kenya imejitolea kushirikiana na nchi nyingine hasa nchi jirani katika kukabiliana na ukuzaji wa madawa ya kulevya ambao alisema mara nyingine unafanikishwa na usafiri wa mpakani.

Kenya inawakilishwa katika kongamano hilo na wizara ya mambo ya ndani, shirikika la kupambana na mihadarati nchini NACADA, bodi ya dawa na sumu na kituo cha ripoti za kifedha.

Opwora ambaye ni katibu wa usimamizi wa masuala ya kitaifa katika idara ya usalama wa ndani katika wizara ya mambo ya ndani nchini alisema vita dhidi ya maandalizi na ukuzaji wa madawa ya kulevya na mihadarati vimefanikishwa nchini na utekelezaji wa sheria.

Sheria hiyo ya kudhibiti mihadarati na madawa ya kulevya ya mwaka 1994 na ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2022, imepiga marufuku ukuzaji wa mimea fulani kama vile bhangi.

Opwora alisema regular uangalizi wa kila mara nyanjani na kuharibu mimea iliyopigwa marufuku na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaopatikana wakikiuka sheria ni sehemu ya mikakati ambayo serikali ya Kenya imekuwa ikitumia ili kuhakikisha kutokomezwa kwa mihadarati na madawa ya kulevya.

Alisema pia kwamba shirika la NACADA limekuwa likitekeleza jukumu lake na limekuwa likitagusana na jamii na kuwahamasisha kuhusu hatari za biashara haramu ya mihadarati na badala yake kuwahimiza kukuza mimea mbadala.

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa NACADA Profesa John Muteti aliyezungumza katika kongamano hilo naye alifafanua kuhusu juhudi za shirika hilo za kuhamasisha umma kuhusu hatari ya kukuza mimea ya madawa ya kulevya.

Muteti alisema kupitia NACADA, Kenya pia inaandaa sera ya kitaifa kuhusu matumizi mabaya ya pombe na mihadarati ambayo inahimiza kuandaliwa kwa mipango inayolenga sio tu ukuzaji wa mimea hiyo bali pia kusimamia maslahi ya makundi yaliyo katika hatari ya kuathirika wakiwemo wanawake na watoto wanaojihusisha na ukuzaji huo.

Huku akikubali kwamba bado yapo mengi ambayo hayajaafikiwa katika vita dhidi ya mihadarati, Opwora alisifia kongamano hilo jijini Abuja akisema ni jukwaa zuri la kujifahamisha yanayohitajika kufanywa nchini Kenya.

Website | + posts