Home Habari Kuu Kenya yatumia mkakati wa sehemu tatu kumaliza tishio la mashambulizi ya kigaidi

Kenya yatumia mkakati wa sehemu tatu kumaliza tishio la mashambulizi ya kigaidi

0

Kufuatia ongezeko la tishio la ugaidi katika eneo la Kaskazini Mashariki na sehemu za Pwani, serikali inaangazia mkakati ambao unalenga kurejesha amani ya kudumu na usalama.

Kando na doria na ufuatiliaji wa kila mara, rasilmali zaidi zimewekezwa katika kuharakisha mageuzi yaliyosubiriwa kwa hamu katika sekta ya usalama.

Mageuzi hayo ni pamoja na kuhakikisha kwamba vikosi vya ulinzi vinapatiwa vifaa kama silaha za kisasa na mavazi ya kujikinga.

Katibu wa usalama wa ndani Dr. Raymond Omollo ambaye alizungumza huko Malindi baada ya kuhutubia kikao cha kamati ya kiufundi ya mageuzi katika idara ya polisi inayoongozwa na aliyekuwa jaji mkuu David Maraga alisema kwamba serikali imejitolea kuharakisha mpango huo ambao utekelezaji wake umepatiwa muda wa miaka miwili.

Alisema kwamba kamati hiyo inayoongozwa na Maraga itapeana ripoti yake kwa Rais William Ruto katika muda wa wiki moja ijayo, kwa lengo la kushughulikia maslahi ya maafisa wa usalama na kuimarisha ufanisi wao kazini.

Omollo aliongeza kwamba wanatizamia kupata mapendekezo muhimu na maalumu kutoka kwa ripoti hiyo ambayo wakiyatekeleza yatasaidia sana kuhakikisha matatizo ya maafisa wa polisi yanashughulikiwa ipasavyo.

Katika bajeti yake ya kwanza ya mwaka 2023/24, Rais William Ruto alitenga shilingi milioni 500 za kutekeleza awamu ya kwanza ya mpango wa kununua vifaa vya kisasa vya maafisa wa usalama.

Chini ya mpango huo, vikosi vya ulinzi vitapokea mavazi mapya ya kujikinga, magari yenye silaha ya kusafirisha maafisa hao, magari ambayo hayaharibiwi na mabomu, ndege zisizoendeshwa na rubani pamoja na helikopta za bunduki ili kuimarisha uwezo wao wa kuepusha na kujibu mashabulizi ya kigaidi.

Vifaa vya kisasa vya mawasiliano pia vitanunuliwa huku maafisa wakipatiwa mafunzo ya kuhakikisha mabadiliko katika namna wanavyofanya kazi na kuimarisha utaalamu.

Katibu Omollo alisema pia kwamba wameimarisha juhudi za kuhakikisha ushirikiano kati ya maafisa wa usalama wa vikosi mbali mbali na jamii katika kujibu tishio hilo la ugaidi ambalo limekumba maeneo hayo kwa muda mrefu.

Mipango ipo ya kuhamasisha umma na wadau wengine kutekeleza majukumu zaidi katika kuzuia na kujibu mashabulizi yanayolenga Kenya.

Omollo anaamini mashambulizi ya kila mara yatamalizwa na hatua hiyo kama ilivyoshuhudiwa awali ambapo maafisa wa usalama wameweza kuzuia mashambulizi kutokana na ushirikiano kati yao na wananchi.

Alisema wanahimiza utamaduni wa maafisa wa usalama kushiriki mazungumzo ya wazi na wadau wengine kama vile jamii za maeneo husika. Alitaja mashirika ya kijamii na viongozi waliochaguliwa akiwahimiza kuchukua hatua ya kuhakikisha wanawasiliana na maafisa wa usalama ili kuzuia mashambulizi ya kigaidi.

Mpango wa kupunguza ukosefu wa usalama na ugaidi katika eneo la kaskazini na pwani yaani Reducing Insecurity and Violent Extremism in Northern and Coastal- REINVENT ni kati ya hatua ambazo zimezaa matunda katika kuhamasisha umma na kuimarisha uthabiti wa jamii na watu binafsi wa kuchukua hatua dhidi ya magaidi na makundi ya uhalifu.

Mpango huo wa miaka mitano unafadhiliwa na UKAid, na unashirikisha mashirika ya serikali na washirika wengine kwa lengo la kuimarisha utendakazi wa maafisa wa polisi.

Website | + posts