Home Habari Kuu Kenya yailaza Tanzania na kutinga fainali ya kipute cha CECAFA U-18

Kenya yailaza Tanzania na kutinga fainali ya kipute cha CECAFA U-18

0

Timu ya Kenya ya chipukizi wenye umri wa chini ya miaka 18 imefuzu kwa fainali ya mashindano ya mwaka huu ya kuwania kombe la CECAFA.

Hii ni baada ya kuilaza Tanzania kwa magoli 4-3 kupitia mikwaju ya penalti wakati wa mchuano wa nusu fainali ya pili uliosakatwa katika uwanja wa Mamboleo katika kaunti ya Kisumu.

Timu zote mbili zilikuwa zimetoka sare tasa katika muda wa kawaida na ziada na kulazimu matuta ya penalti kupigwa ili kuamua mshindi.

Juhudi za wachezaji chipukizi wa timu hizo kujituma kwa udi na uvumba ili kukwepa matuta ya penalti zilikosa kuzaa matunda baada ya timu zote kushindwa kutikisa wavu katika mud wa kawaida na wa ziada.

Hali hiyo iliwasababishia mashabiki mashaka si haba ingawa timu zote mbili zilipata fursa muhimu za kumaliza mchezo mapema.

Kenya sasa itamenyamana na Uganda katika fainali ya mashindano hayo itakayogaragazwa Ijumaa wiki hii.

Hii ni baada ya Uganda kuilaza Rwanda goli moja kwa nunge katika mchuano wa kwanza wa nusu fainali uliosakatwa mapema hii leo.