Home Biashara Kenya yasimamisha uagizaji sukari kutoka nje ya COMESA na EAC

Kenya yasimamisha uagizaji sukari kutoka nje ya COMESA na EAC

Karanja alisema hatua hiyo imetokana na kuimarika kwa uzalishaji wa sukari ya kutosha, huku uzalishaji huo ukitarajiwa kuongezeka maradufu mwaka 2024.

0
Waziri wa kilimo Dkt. Andrew Karanja.
kra

Waziri wa kilimo Dkt. Andrew Karanja, amepiga marufuku uagizaji sukari kutoka mataifa yasiyo wanachama wa soko la pamoja la Kusini na Mashariki mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kupitia kwa taarifa, Karanja alisema hatua hiyo imetokana na kuimarika kwa uzalishaji wa sukari ya kutosha, huku uzalishaji huo ukitarajiwa kuongezeka maradufu mwaka 2024.

kra

“Katika muda wa miaka minne iliyopita, Kenya imezalisha metriki tani 700,000 ya sukari kutoka kampuni 16, na kuongezeka hadi metriki tani 800,000 kufikia mwaka 2022. Uzalishaji wa sukari mwaka 2024 unabashiriwa kupiku kiwango hicho,” alisema Dkt Karanja.

Kulingana na waziri huyo, Kiangazi kilichoathiri mataifa ya COMESA na EAC, kilisababisha Kenya kukubali uagizaji wa sukari kutoka nchi ambazo sio wanachama wa masoko hayo mawili.

Dkt. Karanja alisema uagizaji huo ulilenga kuwakinga wananchi dhidi ya bei ghali ya bidhaa hiyo muhimu.

“Kutokana na kuimarika kwa uzalishaji wa sukari katika nchi za EAC na COMESA, hatua ambayo imesababisha kupungua kwa bei ya sukari, uagizaji sukari kutoka mataifa ambayo sio wanachama wa COMESA na EAC umesitishwa,” alisema waziri huyo.

Aidha waziri huyo alisema taifa hili pia linakabiliwa na uingizaji sukari nchini kinyume cha sheria, hasaa kupitia maeneo ya mipakani, akidokeza kuwa maafisa wa usalama wanakabiliana na hali hiyo.

Website | + posts