Kenya imepongeza hatua zilizopigwa na Rwanda, baada ya taifa hilo kughubikwa na mauaji ya kimbari, huku ikisema itaendeleakuunga mkono nchini hiyo kwa ustawi wa pande hizo mbili.
Hayo yalisemwa na Katibu katika wizara ya mambo ya nje Korir Sing’Oei, aliyeiwakilisha serikali ya Kenya katika makumbusho ya 30 ya mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994.
Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa katika afisi za umoja wa Mataifa eneo la Gigiri, Jijini Nairobi, yaliwaleta pamoja zaidi ya watu 1,000 wakiwemo jamii ya raia wa Rwanda wanaoishi nchini Kenya, maafisa wa serikali ya Kenya, maafisa wa nchi za kigeni, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, marafiki wa Rwanda miongoni mwa wengine.
Akihutubia mkutano huo, katibu Sing’Oei alisema Kenya inasimama kidete na Rwanda pamoja raia wa nchi hiyo, huku Kenya ikijifunza mengi jinsi Kigali ilivyoweza kujinasua katika hali hiyo na kujijenga upya.
“Rwanda ya siku ya leo ni sawia na kioo cha maendeleo, taifa liilobuniwa na maono ya pamoja, kwa kuzingatia mageuzi ya kimsingi,” alisema Sing’Oei.
Matamshi yake yaliungwa mkono na balozi wa Rwanda hapa nchini Kenya Martin Ngoga, alisema mauaji hayo ya Kimbari yanapaswa kuwa kumbukumbu ya kukabiliana na chuki, ubaguzi na migawanyiko iwapo zitaibuka.