Home Habari Kuu Kenya yapiga hatua katika juhudi za kudhibiti sekta ya kamari

Kenya yapiga hatua katika juhudi za kudhibiti sekta ya kamari

0

Kenya imepiga hatua katika harakati za kutafuta kudhibiti sekta ya kamari nchini. Hii ni baada ya jopo lililobuniwa kwa sababu hiyo kufika mbele ya kamati ya bunge kuhusu michezo na utamaduni.

Jopo hilo linaloongozwa na Narendra Naval, lilifika mbele ya kamati hiyo ya bunge kufafanua kuhusu miswada miwili inayolenga kudhibiti sekta ya michezo ya bahati nasibu.

Miswada hiyo ni ule wa kubuni mchezo wa kitaifa wa kamari wa mwaka 2023 na mswada wa kudhibiti sekta ya michezo ya bahati nasibu nchini wa mwaka 2023.

Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa mbunge wa Webuye Magharibi Daniel Wanyama, ilifahamishwa kwamba iwapo sekta hiyo itadhibitiwa, itailetea serikali shilingi bilioni 50 hadi 60 kila mwaka.

Jopo la Narendra Naval, linasisitiza kwamba sheria ya michezo ya kamari ya mwaka 1960 imepitwa na wakati na haishughulikii mabadiliko yanayojiri katika sekta ya kamari kwa sasa.

Mswada wa kudhibiti sekta ya kamari ya mwaka 2023 inatarajiwa kuunda mfumo wa shughuli zote za kamari nchini kupitia kuhakikisha kwamba Wakenya wanacheza michezo ya kamari kwa kuwajibika, kupunguza madhara ya michezo hiyo katika jamii, kuhakikisha uadilifu na haki katika michezo ya kamari iliyo na leseni na kuunda mfumo wa kutatua mizozo ambayo huenda ikatokana na michezo ya kamari.

Mswada wa mchezo wa kitaifa wa kamari wa mwaka 2023 kwa upande mwingine, unalenga kuwezesha serikali kubuni mchezo wa kitaifa wa kamari, kubuni bodi ya kusimamia mchezo huo na hazina ya mchezo huo.

Kulingana na jopo hilo, Kenya ikitekeleza hili, itajiunga na nchi kama Uingereza, Ufaransa, Afrika Kusini na Ghana ambazo zinaendesha michezo ya kamari ya kitaifa.