Home Habari Kuu Kenya yakosoa kauli za Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN

Kenya yakosoa kauli za Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN

0

Kenya imekosoa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Haki za Binadamuu ya Umoja wa Mataifa, UN kuhusiana na maandamano yanayoendelea nchini humo. 

Kupitia msemaji wake Jeremy Laurence, ofisi hiyo ililaani kuenea kwa vurugu wakati wa maandamano ya amani ya Azimio na hatua ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.

“Ripoti zinaashiria kuwa hadi watu 23 wamefariki na makumi kujeruhiwa katika kipindi cha wiki moja iliyopita,” alisema Laurence katika taarifa wiki jana.

Taarifa ambayo Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Alfred Mutua ameitaja kuwa upotoshaji mkubwa.

“Wanazungumzia watu 23, watu hao 23 ni kina nani ambao wanasema walifariki?” Ningependa kuwajua majina yao na wengineo. Wanatupa tu majina na idadi iwe yawe. Hiyo ni tabia mbaya kwa taasisi yenye hadhi kama hiyo,” alisema Dkt. Mutua wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumatano.

“Tunafahamu kuwa vitendo vya vurugu vilivyotekelezwa na wahalifu wachache waliolipwa ambavyo tumeona vimechochewa kisiasa na wachochea vurugu wanaojulikana na kwa hivyo haviwezi vikatajwa kuwa maandamano ya amani kama ilivyodaiwa na msemaji huyo. Hayo si maandamano ya amani kamwe bali ni maandamano ya vurugu huku wahusika wakibeba kila aina ya silaha hatari.”

Dkt. Mutua alizungumza hayo wakati maandamano yaliyoitishwa na muungano wa upinzani nchini humo kuanzia leo Jumatano hadi Ijumaa yakionekana kuzimwa pakubwa.

Isipokuwa visa vya polisi kuwakabili waandamanaji katika mtaa wa Kibera jjijini Nairobi ambayo ni ngome ya kisiasa ya upinzani, baadhi ya sehemu za kaunti za Mombasa na Nakuru, hali ya utulivu ilionekana kushuhudiwa katika sehemu nyingi nchini huku maafisa wa usalama wakishika doria.

Hata hivyo, watu wengi walisalia manyumbani kwa hofu ya kujeruhiwa na wafanyabiashara kufunga biashara zao kwa hofu ya mali zao kuporwa.

Mjini Garissa, baadhi ya wakazi sasa wanatoa wito kwa muungano wa Azimio kufutilia mbali miito yake ya maandamano.

Ingawa wanakiri hali ya maisha imekuwa ngumu zaidi, wanasema maandamano sio suluhu wakiongeza kuwa yatazorotesha hali zaidi.

Dubat Ali Ahmey ni mwenyekiti wa Baraza la Kunadi Mifugo Nchini Kenya. Ametoa wito wa kufanywa mazungumzo kati ya serikali na upinzani.

“Ni wakati wa Rais William Ruto na Raila Odinga kuanza kuzungumza na kukoma kujibizana.”

Kauli sawia zimetolewa na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini humo.

 

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here