Home Habari Kuu Kenya yakosa viwanja kwa mashindano ya kimataifa

Kenya yakosa viwanja kwa mashindano ya kimataifa

0

Kenya inakabiliwa na ukosefu wa viwanja vya kuandaa mashindano ya kimataifa hususan katika mchezo wa riadha na soka.

Hali hii imeleta mfadhaiko mkubwa kwa wachezaji ambao wanalazimika kushiriki mashindano ya kimataifa katika mataifa ya nje, ili kuafikia viwango vinavyo hitajika vya kufuzu.

Chama cha Riadha Kenya kinapanga kuandaa mashindano ya kitaifa kati ya tarehe 15 na 17 mwezi huu.

Hata hivyo kutokana na ukarabati unaoendelea katika viwanja vya Kasarani na Nyayo ambayo ndivyo pekee vinavyoafiki viwango vya kimataifa, mashindano hayo yataandaliwa katika uwanja wa Ulinzi Sports Complex.

Mashindano hayo hayatatumika kufuzu kwa michezo ya Olimpiki jinsi ilivyopangwa awali, hali ambayo inawanyima wanariadha wa humu nchini fursa ya kutimiza muda wa kufuzu kushiriki kwa michezo ya Olimpiki ya Paris Ufaransa.

Hali hii inamaanisha wanariadha wa Kenya watalazimika kushiriki mashindano ya kigeni kutafuta muda wa kufuzu hali inayoongeza gharama kwa taifa na pia wanamichezo.

Miongoni mwa mashindano ambayo wanariadha wanatafuta muda wa kufuzu kwa Olimpiki ni mita 400,mita 800,mita 1500, mita 3000 kuruka viunzi na maji, 5,000 ,mita  10,000 ,matembezi kilomita 20,na mbio za kupokezana kijiti mita 100 kwa wanariadha wanne ,na mita 400 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti.

Timu ya taifa ya soka Harambee Stars imeratibiwa kuwaalika Burundi na Ivory Coast mwezi ujao jijini Nairobi kwa mechi za kundi F kufuzu kwa kombe la Dunia .

Kutokana na kukosekana kwa viwanja vya Nyayo na Kasarani ambavyo vinafanyiwa ukarabati Kenya itabidi ihamishie mechi hizo ugenini .

Uwanja wa kimataifa wa Kasarani ulifungwa yapata miezi mitatu iliyopita ili kufanyiwa uakarabati, huku ule wa Nyayo ukifungwa mapema wiki hii kwa ukarabati kwa minaajili ya  matayarisho ya michuano ya kombe la CHAN mwishoni mwa mwaka huu,na kombe la AFCON mwaka 2027 kwa pamoja na Tanzania na Uganda.