Home Michezo Kenya waitia adabu Somalia michuano ya CECAFA

Kenya waitia adabu Somalia michuano ya CECAFA

0

Timu ya taifa ya kenya imedumisha rekodi ya kushinda mechi zote tatu za kundi A kwenye michuano ya CECAFA kwa wavulana walio chini ya umri wa miaka 18, walipoititiga Somalia magoli 4-1 Ijumaa katika uwanja Bukhungu, kaunti ya kakamega.

Somalia walichukua uongozi kunako dakika ya 19 kupitia kwa Abdihafid Abdi, kabla ya Humprey Aloko kusawazisha dakika ya 25 na Stanley Omondi akaiweka Kenya uongozini dakika tatu baadaye na kuongoza 2-1 kufikia mapumziko.

Katika kipindi pili, Omondi aliongeza bao la dakika ya 66, kisha Aldrine Kibet akahitimisha shughuli kwa bao la nne dakika ya 74.

Katika mchuano mwingine uliochezwa sambamba katika uwanja wa Mamboleo, Rwanda imefuzu kwa nusu fainali kufuatia ushindi wa magoli 3 kwa nunge dhidi ya Sudan.

Kenya wameongoza kundi A kwa alama 9 wakifuatwa na Rwanda kwa alama 6.

Mechi za kundi B zitakamilika Jumamosi Zanzibar, Tanzania, Uganda na Sudan Kusini zikiwa na pointi tatu kila moja.

Rwanda wakichuana na Sudan

Uganda watamenyana na Sudan Kusini katika uwanja wa Mamboleo, Kisumu wakati Tanzania ikimaliza udhia na ndugu zao Zanzibar.

Mechi za nusu fainali zitaandaliwa Jumanne ijayo huku fainali ikipigwa siku ya Ijumaa.