Kenya iko tayari kuandaa mashindano ya dunia ya mbio za Nyika ya shule {International Schools Federation} ISF World Schools Cross Country, tarehe 12 mwezi huu katika uwanja wa Ngong Racecourse.
Kwa mjibu wa Mkurugenzi wa mashindano hayo Barnaba Korir, takriban wanafunzi 461 kutoka mataifa 41 wanatarajiwa kushiriki mashindano hayo ya siku moja .
“Tumepata thibitisho la mataifa 41 ambayo yatashiriki na wanafunzi wote watakuwa 461 kutoka nchi 41,naweza sema kuwa tuko tayari uwanja tumeandaa na tunatarajia wanafunzi kuanza kuwasili tarehe 9 mwezi huu.”akasema Korir
“Tarehe 10 na 11 tutatkuwa na maonyesho mbalimbali kutoka kwa wanafunzi, kama njia ya kutangamana na kisha tarehe 12 ndiyo siku ya mashindano.” Korir akaongeza
Kikosi cha Kenya kinachowajumuisha wanariadha 61 kimeimarisha mazoezi ya kambi mjini Ngong baada ya kuteuliwa kutoka kwa michezo ya shule .
Kocha wa Kenya Robert Ng’isirei amesema vijana wake wanaendelea na mazoezi vyema licha ya kutatizwa na mvua kubwa inayonyesha eneo la Ngong.
“Mvua kubwa inayonyesha hapa Ngong imekuwa tatizo kwetu ingawa inabidi tutafute mbinu mbadala ya kufanya mazoezi,hata hivyo mazoezi yanaendelea vizuri kambini na morali ya wachezaji iko juu.”amesema kocha Ng’isirei
Mashindano hayo yanaandaliwa na wizara ya elimu kwa ushirikiano na chama cha riadha Kenya.
Kenya inaandaa makala hayo ya pili ya mashindano ya dunia ya mbio za nyika kwa shule ikiwa nchini ya pili ya Afrika, kupewa jukumu hilo baada ya Morocco iliyokuwa mwenyeji mwaka 2000.
Mashindano hayo yatakuwa ya vitengo vya wavulana na wasichana walio chini ya umri wa miaka 12,wavulana na wasichana chini ya umri wa miaka 15 na wavulana na wasichana wasiozidi umri wa miaka 18.
Baadhi ya mataifa yalitoa ithibati kushiriki ni Ethiopia, Chile, Uganda, Namibia, New Zealand, Turkey, Luxembourg, Tanzania, Italy, England, Ireland, Saudi Arabia, Nigeria na China.