Home Habari Kuu Kenya na DRC ni washirika wakuu Afrika Mashariki, asema Mudavadi

Kenya na DRC ni washirika wakuu Afrika Mashariki, asema Mudavadi

0
Waziri Mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi (Kushoto), na Rais wa DRC Ferlix Tshisekedi (Kulia).

Kenya imekariri kwamba itaendelea kuzingatia uhusiano wa karibu ulioko baina yake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi, aliyewasilisha ujumbe maalum wa rais William Ruto kwa rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha uhusiano baina ya mataifa haya mawili kwa ajili ya ufanisi wa raia wake.

Mudavadi aliyekuwa akiongea mjini Kinshasa  baada ya kukutana na rais Tshisekedi, aliongeza kwamba Kenya imejitolea kuboresha uhusiano wa kibiashara na kiusalama baina yake na DRC.

Mudavadi ambaye yuko nchini DRC kwa ziara rasmi ya  siku moja, alisema kwamba katika juhudi za kuimarisha ufanisi na ushirikiano miongoni mwa wanachama wa jumuiya ya afrika mashariki, mataifa wanachama lazima yajitolee kushirikiana katika sekta zenye manufaa kwao.

Alisema Kenya inamshukuru Rais Tshisekedi kwa kuingilia kati na kusuluhisha utata uliozingira kukamatwa kwa maafisa wawili wa shirika la ndege la Kenya Airways, akisema swala hilo limetatuliwa kikamilifu.

“Tuko hapa kumshukuru Rais na kusisitiza kuwa ushirikiano wetu ni mkubwa. Nawahakikishia raia wa Kenya kwamba kuna ujumbe mzuri kwa Rais William Ruto,” alisema Mudavadi.

Mudavadi alikuwa ameandamana na katibu wa uchukuzi Mohammed Daghar na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la ndege la Kenya Airways Allan Kilavuka miongoni mwa wengine.