Home Habari Kuu Kenya na China zasaini makubaliano ya biashara ya mabilioni ya pesa

Kenya na China zasaini makubaliano ya biashara ya mabilioni ya pesa

0

Kenya na China zimesaini makubaliano ya biashara yenye kima cha shilingi bilioni 63 katika nyanja za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, ICT, afya na uhandisi.  

Makubaliano hayo yalisainiwa kati ya Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda cha Kenya na kile cha China katika juhudi za kuongeza biashara kati ya nchi hizo mbili.

Wakizungumza jijini Beijing wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo, Rais wa Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda cha Kenya Dkt. Eric Rutto na mwenzake wa China Chen CongCong walisititiza haja ya kuhamasisha biashara kwa manufaa ya raia wa nchi hizo mbili.

ConCong alielezea mashaka kuwa kuna ukosefu wa uwiano wa biashara kati ya Kenya na China, akiongeza kuwa juhudi zinapaswa kufanywa kurekebisha hali hiyo.

“Kuna haja ya kuweka jukwaa la kawaida la biashara kuangazia mashaka ya wafanyabiashara wanaohudumu katika nchi zote mbili,” alisema CongCong.

Kwa upande wake, Rutto alisema Kenya imeanzisha ofisi ya kudumu ya uwakilishi nchini China ili kulinda uwekezaji wa Kenya.

“Kenya pia imeongeza juhudi za kuuza nchini China bidhaa zake za kilimo ikiwa ni pamoja na kahawa, makadamia na asali miongoni mwa bidhaa zingine kama sehemu ya jitihada za kuhamasisha biashara kati ya nchi zetu,” alisema Rutto.

Wawekezaji wa China walio tayari kuwekeza katika eneo la Konza Technopolis ni pamoja na kampuni ya Uhandisi wa Umme ya Inner Mongolia Mingxu Electric, Dongfeng Venucia Automobile, Guangdong Qiya Exhibition, Gaochuang Import and Export na kampuni ya tiba ya Zhende miongoni mwa zingine.

Rais William Ruto aliyehudhuria mkutano wa uwekezaji kati ya Kenya na China alisema serikali yake imeweka mazingira mwafaka kuwezesha biashara kunawiri.

“Sababu inayoifanya Kenya kuwa bora kwa biashara ni tuna soko kubwa, uwekezaji unalindwa, sisi ni nchi ya kidemokrasia na watu wetu wanafanya kazi kwa bidii na hivyo kuna wingi wa rasilimali watu,” alisema Rais  Ruto.

 

 

Website | + posts