Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi ametoa ahadi kwa vijana kwamba serikali ya Kenya Kwanza imedhamiria kutoa fursa zitakazohakikisha wanajiendeleza kimaisha.
Amewasifia vijana humu nchini na akisema wameendelea kudhihirisha kuwa wana uwezo wa kukuza maendeleo kwa jinsia wanavyofuatilia hali ya mambo kwa makini zaidi.
“Vijana wetu wa kiume na kike wameendelea kudhihirisha kwamba wana uwezo wa kujenga nchi iliyostawi kwa kuzingatia umakini wao kwa ustawi wa taifa lao,” alisema Mudavadi ambaye pia ni Kinara wa Mawaziri.
“Kwa nguvu, shauku na jitihada zao, kile vijana wanahitaji ni fursa za kujiendeleza na kama serikali ya Kenya Kwanza, hiyo ndio ajenda yetu kuu.”
Matamshi yake yanakuja wakati Kenya ikijiunga na ulimwengu kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani leo Jumanne.
Kulingana na data za Umoja wa Mataifa, nusu ya watu wote duniani wana umri wa miaka 30 kurudi chini.
Maudhui ya mwaka huu ya Siku ya Vijana Duniani ni “Kutoka Kubonyeza hadi Maendeleo: Fursa za Kidijitali kwa Vijana kwa ajili ya Maendeleo Endelevu.