Home Habari Kuu Kenya kutumia uhusiano wake na Iran kupanua biashara

Kenya kutumia uhusiano wake na Iran kupanua biashara

Rais Ruto aliashiria kwamba Kenya pia itatumia utajiri wa teknolojia na uvumbuzi wa nchi hiyo ya Asia Magharibi kwa maendeleo yake.

0
Rais William Ruto na mwenzake wa Iran Ebrahim Raisi, katika Ikulu ya Nairobi. Picha/Hisani.

Kenya itatumia vyema uhusiano wake imara na Iran ili kupanua biashara.

Rais William Ruto alisema kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili bado kiko chini lakini kuna uwezekano wa kukua.

Alieleza kuwa Kenya na Iran zitaweka utaratibu utakaoongeza zaidi kiwango cha chai, kahawa na nyama inayouzwa nje ya nchi.

“Hii italeta usawa wa biashara unaotarajiwa ambao kwa sasa umeegemea upande wa Iran.”

Aliyasema hayo leo Jumatano katika Ikulu ya Nairobi baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Iran Ebrahim Raisi.

Ruto aliashiria kwamba Kenya pia itatumia utajiri wa teknolojia na uvumbuzi wa nchi hiyo ya Asia Magharibi kwa maendeleo yake.

Alidokeza kwamba kuanzishwa kwa Jumba la Ubunifu na Teknolojia la Iran mjini Nairobi kutatoa jukwaa mwafaka kwa biashara za Iran na Kenya.

“Hii ni njia bunifu ya kuwezesha makampuni kupata teknolojia, ujuzi na taarifa za Iran.”

Rais Ruto alieleza kuwa Kenya na Iran ziko katika maeneo ya kimkakati yanayozifanya kuwa mahali muhimu kwa kuingia katika kanda zao.

“Tutalenga kutumia faida hii ya kipekee kwa ustawi wetu,” alisema Rais.

Kutokana na maingiliano ya mara kwa mara, Rais Ruto alisema kuwa Kenya na Iran zimetia saini zaidi ya mikataba na makubaliano 22.

Makubaliano hayo yamekuwa na umuhimu katika ushirikiano katika maendeleo, elimu, ufadhili wa masomo, miundombinu, afya, maji, uvuvi na kilimo.

Wakati wa mkutano wao, Ruto na Raisi walishuhudia kutiwa saini kwa makubaliano na mikataba mipya katika nyanja za kilimo, mifugo, utamaduni na urithi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, uvuvi, makazi, maendeleo ya mijini na miji mikuu.

Rais Ruto alisifu uungwaji mkono wa Iran katika afya, akiitaja kuwa hatua muhimu kuelekea kuafikia utoaji wa Huduma Bora ya Afya kwa Wote nchini Kenya.

Rais Raisi alipongeza kujitolea kwa Kenya kuweka mazingira rafiki kwa biashara za kigeni.

Alisema makampuni zaidi ya Iran yataanzisha shughuli zake nchini, na hivyo kufungua njia yao ya kufikia masoko ya Afrika Mashariki, Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) yaliyo na zaidi ya watu bilioni 1.4.

“Uhusiano wa Kenya na Iran unaweza daima kuimarishwa kwa manufaa yetu,” alisema wakati wa mkutano na wanahabari.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here