Home Habari Kuu Kenya, Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati kushirikiana dhidi ya ugaidi

Kenya, Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati kushirikiana dhidi ya ugaidi

0

Mataifa ya Kenya, Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati yatashirikiana katika kupigana na ugaidi na ukosefu wa usalama barani humu.

Rais William Ruto alisema nchi hizi tatu zimejitolea kutafuta na kuafikia amani ya kudumu na udhabiti katika bara Afrika.

Kulingana naye, watakuwa wakijuzana taarifa za kijasusi na kuwa na msimamo sawa katika majukwaa ya kimataifa ili kuimarisha ajenda ya amani Afrika.

Kiongozi wa taifa alisema nchi hizo zitashirikiana kwa karibu kupambana na itikadi kali na ugaidi ili kuafikia amani, usalama na udhabiti.

“Nchi zetu zinahitaji kushirikiana kutafuta suluhu mwafaka kwa matatizo sawia yanayosibu amani ulimwenguni na katika kanda hii.” alisema Rais.

Alikuwa akizungumza Jumapili alipokutana na marais Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Denis Sassou N’Guesso wa Congo mjini Oyo, nchini Congo.

Viongozi hao wamejitolea kuboresha ushirikiano kati ya mataifa haya matatu na kuimarisha biashara katika bara Afrika.

Rais Ruto alisema wako macho kuchunguza fursa zinazochipuza na zile ambazo hazijatumiwa za kibiashara kwa manufaa ya wananchi.

“Huu ndio wakati wa Afrika kufanya biashara na Afrika na Kenya iko ange kushirikiana na Jamhuri ya Afrika ya Kati na Congo kuafikia hili.” aliongeza Rais Ruto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here