Home Kimataifa KeNHA yapendekeza ada kwa wanaotumia barabara fulani kuu nchini

KeNHA yapendekeza ada kwa wanaotumia barabara fulani kuu nchini

0
kra

Mamlaka ya kitaifa inayosimamia barabara kuu nchini -KeNHA imetangaza kwamba majadiliano yanaendelea kuhusu kuanzisha utozaji ada watumizi wa barabara fulani kuu nchini.

Barabara ilizotaja ni pamoja na ile kuu ya kuelekea mjini Thika, barabara kuu ya kusini mwa Nairobi, barabara kuu ya kutoka Nakuru kuelekea Mau Summit, barabara kuu ya kutoka Kenol-Sagana-Marua, barabara kuu ya kusini mwa Mombasa na barabara kuu ya Dongo Kundu.

kra

Wakenya wamehakikishiwa kwamba watapata fursa ya kutoa maoni kuhusu suala hilo inavyohitajika kikatiba kabla ya ada hizo kuanza kutozwa.

Kulingana na KeNHA sera itabuniwa ambayo itatoa mwelekeo wa barabara zitakazotolewa ada na kwamba mamlaka hiyo imejitolea kuhusisha uwazi na ujumuishaji katika mchakato mzima huku ikihusisha wananchi.

Wakati akihudumu kama waziri wa uchukuzi na barabara, Kipchumba Murkomen aligusia suala hili la kutoza ada watumizi wa barabara fulani nchini kwa lengo la kukusanya mapato ya ujenzi wa barabara zaidi nchini.

Imebainika kwamba utozaji ada watumizi wa barabara upo kwenye mpango makhsusi wa KeNHA wa mwaka 2023 hadi 2027 ambao unaendelea kutekelezwa kwa sasa.

Pendekezo hilo hata hivyo lilivutia ukosoaji kutoka kwa wananchi wakati lilitangazwa awali. Wananchi wanahisi kwamba ushuru unaokusanywa na serikali unatosha kukarabati na kujenga barabara kote nchini.