Home Habari Kuu KeNHA: Hatujalitenga eneo la Nyanza katika ujenzi wa barabara

KeNHA: Hatujalitenga eneo la Nyanza katika ujenzi wa barabara

0

Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Barabara Kuu Nchini, KeNHA imekanusha madai kuwa imelitenga eneo la Nyanza katika mipango yake ya ujenzi wa barabara.

Hii ni baada ya zabuni zilizotangazwa na mamlaka hiyo Agosti 15, 2003 za ujenzi wa barabara mbalimbali kwa robo ya kwanza na ya pili ya mwaka wa fedha wa 2023/24 huku baadhi wakiibua mashaka kuwa tangazo hilo halikuzijumuisha barabara za eneo la Nyanza.

Katika taarifa, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano wa KeNHA Samwel Kumba anasema ni muhimu kubaini kuwa kandarasi za ujenzi hutolewa kwa vipindi tofauti kulingana na vipindi vya kandarasi za miradi inayotekelezwa.

“KeNHA ilitangaza zabuni za ujenzi wa barabara kwa robo mwaka za tatu na nne katika mwaka wa fedha wa 2022-2023. Jumla ya zabuni 14 zilitangazwa kwa ajili ya kazi za ujenzi katika eneo la Nyanza zenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 1.5,” inasema KeNHA katika taarifa.

Mamlaka hiyo imetaja barabara kama vile ile ya Muhuru – Masara Road na Sindo – Nyagwethe – Kiabuya kuwa miongoni mwa zile  ambazo zimepangiwa kufanyiwa ukarabati katika eneo la Nyanza.

Aidha, shilingi milioni 833 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Mamboleo – Miwani – Chemelil – Muhoroni (Kipsitet) na shilingi milioni 260 kwa ukamilishaji wa barabara ya Kisumu Boys – Mamboleo Road, Dhogoye Bridge, na Ahero na makutano ya Kericho.