Home Kaunti KEMRI yatakiwa kutafiti sumu ya nyoka huko Nandi

KEMRI yatakiwa kutafiti sumu ya nyoka huko Nandi

Wakaazi wa eneo la Chemase na wauguzi katika kaunti ya Nandi wataka shirika la KEMRI lifungue kituo cha utafiti ili kutambua aina ya nyoka ambao wanauma wenyeji na kutafuta suluhisho.

Wakizungumza katika hafla ya kutolewa kwa dawa kwa zahanati tano lokesheni ya chemase eneo bunge la Tindiret wakaazi hao waliomba shirika la utafiti wa kimatibabu KEMRI wafungue kituo cha utafiti wa sumu za aina mbali mbali za nyoka ambao wamekuwa wakiuma wakaazi wa maeneo hayo.

Zahanati tano za Chemase , Chepswerita, Kibongwa , Kibisen na Chemursoi zilipokea dawa za thamani ya zaidi ya shilingi elfu mia moja hamsini, kila zahanati ikipokea dawa za shilingi elfu 30, zilizotolewa kwa udhamini na kampuni ya uchimbaji migodi ya dhahabu Karebe.

Muuguzi Amos Barno na mwenyekiti wa kamati ya ushirikiano na wananchi wa sehemu hiyo Henry Muge walishukuru kampuni hiyo ya Kuchimba migodi ya Karebe kwa kushirikiana na gatuzi la Nandi kuhakikisha afya bora kwa wakaazi.

Walisema kampuni ya Karebe hutoa dawa za thamani ya shilingi elfu 30, kila mwezi kusaidia zahanati hizo. Zahanati ya Chemase iliyofunguliwa Januari 19, 1969 na aliyekuwa waziri wa uchumi na mipango wa maendeleo Tom Mboya miezi kadhaa kabla yakupigwa risasi, inahudumia zaidi watu 10,000 na inahitaji upanuzi wa dharura ili kuwezesha wakaazi wa eneo hilo kupata matibabu ya ubora wa hali ya juu.

Barno ambaye pia ni msimamizi wa wahudumu ya afya katika zahanati hiyo, aliomba wahisani na serikali ya ugatuzi kusaidia kuweka vifaa vya kisasa kama vile mitambo ya xray humo, ili kukimu mahitaji ya wagonjwa.

Alimsihi Gavana wa kaunti ya Nandi Stephen Sang atoe kipaumbele kwa maswala ya afya.

Gilbert Terer wa kampuni ya Karebe alisema kampuni hiyo hutoa msaada wanaoishi karibu kulingana na maombi yao.

Website | + posts
Kimutai Murisha
+ posts