Home Biashara KCAA yakanusha madai kwamba huenda ndege ya KQ ingehusika katika ajali

KCAA yakanusha madai kwamba huenda ndege ya KQ ingehusika katika ajali

Kupitia kwa taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano, KCAA ilisema hatua ya kuzunguka angani kwa ndege ni jambo la kawaida kwa lengo la kuimarisha usalama.

0
Afisi za halmashauri ya safari za ndege nchini, KCAA.

Halmashauri ya kusimamia safari za ndege hapa nchini (KCAA), imepuuzilia mbali madai kwamba ndege moja ya shirika la ndege la Kenya Airways huenda ingehusika katika ajali.

Kulingana na halmashauri hiyo ya KCAA, ripoti kwamba ajali ingetokea ikihusisha ndege ya shirika la Kenya Airways yenye nambari KQ101 iliyotoka katika uwanja wa ndege wa Heathrow Jijini London tarehe nane mwezi Septemba, ni za kupotosha.

Kupitia kwa taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano, KCAA ilisema hatua ya kuzunguka angani kwa ndege ni jambo la kawaida kwa lengo la kuimarisha usalama.

“Katika siku chache zilizopita, habari za kupotosha zimesambaa katika mitandao ya kijamii, zikidai huenda ajali ya ndege ingetokea katika uwanja wa JKIA,” ilisema taarifa ya KCAA.

“Hatua ya ndege nambari KQ101 kufanya mzunguko angani, ni jambo la kawaida wakati ambapo barabara ya kutua kwa ndege inatumika. Hakuna wakati ambapo usalama wa ndege hiyo na abiria wake ulikuwa hatarini,” iliongeza taarifa ya KCAA.

Halmashauri hiyo iliwahakikishia abiria usalama wa safari zao na oparesheni katika uwanja wa ndege.

Website | + posts