Home Habari Kuu KBC, FKF zasaini mkataba wa kurusha mubashara mechi za ligi kuu

KBC, FKF zasaini mkataba wa kurusha mubashara mechi za ligi kuu

0

Shirika la utangazaji nchini, KBC limesaini mkataba wa kupeperusha mubashara mechi za ligi kuu nchini Kenya, FKF bila malipo kuanzia mwishoni mwa juma hili kwa kima cha  shilingi milioni 119.

Mkataba huo utashuhudia  runinga ya KBC na idhaa zote za KBC zikipeperusha mechi  bila malipo kwa watazamaji na wasikilizaji.

Akitangaza mkataba huo, Waziri wa Michezo Ababu Namwamba amekariri kuhakikisha pia ligi kuu ya soka ya kina dada inapeperushwa kwenye runinga ya KBC hivi karibuni.

Namwamba pia ametoa changamoto kwa FKF kuwa na uwajibikaji, usimamizi bora na uwazi ili kuwavutia wafadhili, hali itakayohakikisha wachezaji wanalipwa donge nono.

Waziri pia amezionyoa timu zinazoshiriki ligi kuu ya FKF kujiepusha na visa vya uhuni wakati wa mechi hali ambayo imesababisha uharibifu wa mali na kuchangia mashabiki kukwepa kuhudhuria mechi uwanjani.

Waziri wa Habari na Mawasiliano Eliud Owalo, aliyeshuhudia uzinduzi huo, alipongeza hatua hiyo akisema itachangia kueneza ukuzaji wa vipaji vya soka nchini.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KBC Samuel Maina alitoa hakikisho la kuendelea kutoa burudani la kipekee la michezo kwa watazamaji kote nchini.

Kulingana na mkataba huo, KBC itapeperusha mubashara mechi kadhaa za ligi hiyo kuanzia mwishoni mwa juma hili kupitia kwa runinga ya KBC Channel 1 na idhaa zote za redio.

Website | + posts