Home Habari Kuu KBC na FKF wazindua mkataba wa ushirikiano

KBC na FKF wazindua mkataba wa ushirikiano

0

Shirika la utangazaji nchini, KBC na shirikisho la soka nchini, FKF yamezindua mkataba wa kupeperusha michuano yote ya ligi kuu nchini.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mkataba huo, kaimu mkurugenzi mkuu wa KBC Samuel Maina alielezea kwamba chini ya mkataba huo, mechi za ligi kuu zitapeperushwa na runinga ya KBC na vituo vyake 13 vya redio.

Alisema hakuna Mkenya anastahili kukosa kuburudika na mechi hizo za ligi ya nyumbani katika sehemu zote za nchi na kwa hilo, runinga ya KBC inatimiza kauli mbiu yake ya kuwa mshirika wa kweli katika spoti.

Maina alishukuru serikali ya Rais William Ruto kwa kutoa fedha kwa shirika la KBC kufadhili mpango wake wa uboreshaji huku akiiomba isaidie KBC kupata haki za kupeperusha mashindano ya AFCON mwaka 2024 na yale ya Olimpiki mwaka 2024.

Rais wa FKF Nick Mwendwa kwa upande wake alielezea tofauti iliyopo kati ya mkataba na KBC na ule wa awali na Azam TV.

Mkataba wa Azam ni wa vituo vya runinga vya kulipiwa ilhali wa KBC ni wa vituo vinavyopatikana bila malipo.

Mkataba wa shirika la KBC na FKF ni wa dola laki 7.5 kwa runinga na dola laki 5 kwa redio.

Mikataba ya Azam na KBC itawezesha kila timu inayoshiriki ligi kuu kupata shilingi milioni 10 kwa mwaka huku wakufunzi wa ligi ya wanawake na ile ya NSL wakipokea malipo.

Kuhusu timu inayoibuka mshindi mwishoni mwa msimu, Mwendwa alielezea kwamba itapata zawadi ya shilingi milioni 5, huku timu nyingine 17 zikigawiwa shilingi milioni 11 kulingana na msimamo katika ligi.

Website | + posts