Shirika la Utangazaji nchini Kenya, KBC litaboresha ushirikiano kati yake na Shirika Kuu la Utangazaji nchini China, CMG ili kuhakikisha masuala yanayohusu nchi hizo mbili yanaangaziwa kwa mapana na marefu kwa manufaa ya raia.
Mashirika ya KBC na CMG yamekuwa na ushirikiano tangu jadi ambao umesababisha vipindi vya CMG kurushwa kwenye runinga na redio za KBC.
Kwa mfano, Ifahamu China ni kipindi maarufu kinachoangazia masuala mbalimbali nchini China kinachorushwa kwenye runinga ya KBC Channel 1.
Chini ya ushirikiano ulioboreshwa zaidi, KBC itaangazia mambo yanayojiri katika nyanja mbalimbali nchini China kama vile sayansi na teknolojia, uchukuzi, utamaduni na uendelezaji wa miundombinu, wakati CMG pia ikiangazia hatua zinazopigwa na Kenya na Afrika kwa jumla katika nyanja mbalimbali kama vile ustawishaji wa miundombinu muhimu kama reli za kisasa na biashara.
“Kumekuwa na changamoto ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kuiangazia China kwa njia hasi, na pia kuchora taswira ya bara la Afrika kuwa kitovu cha changamoto si haba kama vile vita, njaa, magonjwa na kadhalika,” amesema Han Mei, Mkurugenzi wa CMG Swahili.
“Tunaposafiri Afrika, tunapata hali ni tofauti kabisa. Natumai ushirikiano kati ya CMG na KBC na vyombo vingine vya habari vya Afrika utasaidia kuchora taswira halisi ya hali ilivyo nchini China na barani Afrika.”
China ni nchi ya pili iliyokua kiuchumi zaidi duniani na imekuwa ikipania kuongeza ushirikiano kati yake na nchi za Afrika katika nyanja mbalimbali.
Mathalan, siku chache zilizopita, nchi hiyo ilikuwa mwenyeji wa Kongamano la Ushikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) lililoadaliwa mjini Beijing.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi 53 kutoka nchi za Afria akiwemo Rais Wiliam Ruto wa Kenya.
Wakati wa kongamano hilo, China iliahidi msaada wa zaidi ya dola bilioni 50 kwa lengo la kuzifanya nchi za Afrika kuwa za kisasa.
Msaada huo unahusisha nyanja mbalimbali kuanzia kwa miundombinu, kilimo na hata biashara.
Katika hotuba yake, Rais Xi Jinping wa China alisema mtazamo wa nchi za Magharibi kwa usasa “umesababisha mateso makubwa kwa nchi zinazoendelea.”
“Jitihada za pamoja za China na Afrika kuelekea usasa utaanzisha wimbi la usasa katika nchi za Global South,” Rais Xi aliwaambia washiriki wa kongamano hilo.
Na wakati China ikiimarisha zaidi ushirikiano kati yake na nchi za Afrika, CMG ipo mbioni kuimarisha zaidi ushirikiano kati yake na vyombo vya habari vya Afrika.
Ili kuweka bayana azimio hilo, CMG, Agosti 31, 2024, Ilizindua Hafla ya Mkakati wa Ushirikiano kati yake na Vyombo vya Habari vya Afrika Mashariki mjini Beijing.
Hususan, CMG inalenga kuangazia kwa wigo mpana masuala yote yanayojiri katika pande zote mbili kupitia majukwaa yake ya uenezaji habari kama vile runinga, redio na mitandao ya kijamii, wakati masuala hayo pia yakiangaziwa katika vyombo vya habari washirika kupitia ushirikiano huo.
Shirika hilo linaiona hatua hiyo kama itakayosaidia kukabiliana na habari za upotoshaji ambazo mara nyingi huenezwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi dhidi ya China na bara la Afrika kwa ujumla.
Wakati nikiwa mjini Beijing, nilipata pia fursa adimu ya kuzungumza na Gao Wei ambaye ni Makamu Rais wa Shirika la CGTN ambaye pia ni Meneja Mkurugenzi wa CCTV+, na pia Li Xia ambaye ni Naibu Meneja Mkuu Mtendaji wa Shirika la Habari la CCTV Video News.
Wakati wa mkutano huo, Gao na Li waliahidi kukuza ushirikiano zaidi na KBC hasa katika masuala ya dijitali ambapo watachangia maudhui kama vile video zinazozungumzia masuala ya China zitakazochapishwa kwenye mitandao ya KBC na vipindi kurushwa kwenye runinga ya KBC Channel 1.
Pia, wataisaidia KBC kupata vifaa vya kisasa vitakavyosaidia kuboresha utenda kazi wa shirika hilo la umma mbali na kutoa mafunzo yanayohitajika kwa wafanyakazi wake ili kunoa makali yao.
Kwa upande mwingine, wawili hao waliahidi kufanya kila wawezalo kusaidia ukusanyaji wa taarifa humu nchini zitakazorushwa kwenye vyombo vya habari vya China, wakati pia wakiisaidia KBC kupiga hatua katika matumizi ya akili mnemba, yaani Artificial Intelligence (AI) katika utendaji kazi wake.
CMG ni shirika ambalo lilianzishwa mnamo mwaka wa 2018 kwa kuunganisha Radio China Kimataifa (CRI), Televisheni ya Taifa la China (CCTV) na Radio ya Taifa la China (CNR).
CMG hurusha matangazo yake kote duniani kwa kutumia lugha 80 ambazo zinajumuishwa chini ya CGTN.
CGTN ni kitengo kinachorusha matangazo nje ya China kwa kutumia lugha za kigeni.
Kwa upande mwingine, CGTN Kiswahili, almaarufu CRI Kiswahili ilianzishwa mnamo mwaka wa 1961. Idhaa hiyo inawafikia watu wote wanaozungumza lugha ya Kiswahili kupitia FM radio, tovuti, programu ya Cheche na pia mitandao ya kijamii.