Serikali ya kaunti ya Mombasa imetangaza kuwa imelipa madeni yote iliyokuwa ikidaiwa.
Gavana wa kaunti hiyo Abdulswamad Nassir, alithibitisha hayo alipofika mbele ya kamati ya bunge la Seneti kuhusu uhasibu wa pesa za umma.
Maseneta walimpongeza gavana huyo kwa hatua hiyo, ikizingatiwa kwamba kaunti kadhaa bado hazikamilisha ulipaji wa madeni yao.
“Mombasa inafurahia kukamilisha mwaka wa kifedha bila kudaiwa madeni yaliyokuwepo tangu tulipochukua usukani,” alisema Gavana huyo huku akimiminiwa sifa na Seneta wa Isiolo Fatuma Dullo na yule wa Nyandarua Robert Methu.
Maseneta hao wawili pia walimpongeza Gavana Nassir kwa usimamizi bora wa kifedha unaoshuhudiwa katika kaunti hiyo.
Aidha bunge la Seneti lilihakikishia kaunti ya Mombasa kuwa litalinda ugatuzi kwa vyovyote vile, jinsi ilivyoratibiwa katika katiba ya mwaka 2010.
Gavana Nassir alichukua fursa hiyo kufafanua kuhusu pendekezo lake la usajili wa mali katika kaunti hiyo, kwa lengo la kuongeza ukusanyaji ushuru.
Usajili uliopo ulifanywa mwaka 1991 na hauna dhamani ya mali ya sasa katika kaunti hiyo, hii ikimaanisha kuwa kaunti hiyo inapoteza mapato ambayo yangeimarisha utoaji wa huduma.
Wakati wa kampeni za uchaguzi, Gavana huyo aliwaahidi wakazi wa Mombasa kwamba atabuni serikali yenye uwajibikaji, kuaminika na iliyoa na uwazi.
“Nitaendelea kuhakikisha serikali iliyo na uwazi na inayoshughulikia matatizo ya watu wetu,” alisema Gavana huyo.