Home Kaunti Kaunti ya Kajiado yapokea ambulensi za pikipiki

Kaunti ya Kajiado yapokea ambulensi za pikipiki

Pikipiki hizo zitakuwa katika hospitali za kaunti ndogo za Kajiado Kusini, Magharibi, mashariki na ya kati.

0

Ni afueni kwa kina mama wajawazito katika sehemu za mashambani kaunti ya Kajiado, kwani watapokea huduma za matibabu kwa urahisi baada ya kuanzishwa kwa ambulensi za pikipiki.

Mpango huo wa Eezer kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Kajiado kupitia kwa mpango kwa jina ‘Together Together’, unatoa huduma hizo za kuwabeba wagonjwa kwa pikipiki na utatoa huduma za matibabu kwa bei nafuu.

Akiongea alipopokea pikipiki 15 kutoka kwa mpango wa Eezer, afisa mkuu wa afya wa serikali ya kaunti hiyo Alex Kilowua alisema pikipiki hizo za kusafirisha wagonjwa zitasaidia pakubwa kupunguza vifo vya kina mama wajawazito.

Kilowua alisema pikipiki hizo zitakuwa katika hospitali za kaunti ndogo za Kajiado Kusini, Magharibi, Mashariki na ya Kati.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Eezer Lars Klingsbor alisema lengo lao ni kuanzisha uchukuzi salama, wa haraka na wa bei nafuu  kwa kina mama wajawazito  na kuwa na pikipiki  3,000 barani Afrika kufikia mwaka 2030.

“Licha ya kuwa tunajizatiti kufanikisha mpango huu, changamoto kuu ni kwamba kaunti hii inahitaji ambulensi za pikipiki 115 zaidi,” alisema Klingsbor.

Kulingana na Hazina ya Umoja wa Mataifa kuhusu Idadi ya Watu, UNFPA, idadi ya wanawake ambao hufariki kutoka na visa vya uja uzito ni 335 kati ya wanawake 100,000 ambao hujifungua nchini Kenya.

Website | + posts
KNA
+ posts