Home Burudani Katy Perry auza muziki wake

Katy Perry auza muziki wake

0
Katy Perry

Katheryn Elizabeth Hudson, maarufu kama Katy Perry ndiye mwanamuziki wa hivi punde zaidi kuuza katalogi ya muziki wake.

Jumatatu Septemba 18, 2023, kampuni ya usimamizi wa mali iitwayo Carlyle Group, ilitangaza kwamba mwanamuziki Katy Perry alikuwa ameuza katalogi ya muziki wake kwa kampuni ya Litmus Music.

Perry aliuza hakimiliki ya muziki aliotoa kati ya mwaka 2008 na 2020 kwa Dola Milioni 225.

Kazi alizouza mwanamuziki huyo ni pamoja na albamu tano alizoandaa na kampuni ya Capitol Records ambazo ni “One of the Boys” ya mwaka 2008, “Teenage Dream” ya mwaka 2010, “Prism” ya mwaka 2013, “Witness” ya mwaka 2017 na “Smile” ya mwaka 2020.

Hank Forsyth mmoja wa waanzilishi wa kampuni ya Litmus Music ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo alisema muziki wa Perry ni muhimu katika utamaduni wa ulimwengu na wanafurahia kushirikiana naye.

Mwenzake wa kampuni ya Carlyle, Matt Settle alisema, “Tunaamini hili ni dhihirisho la uwezo wa kundi hili kushirikiana na wasanii wakubwa ulimwenguni. Nyimbo za Katy zimeafikia mauzo ya kiwango cha juu na kuathiri utamaduni wa wengi ulimwenguni.”

Wasanii wakubwa ulimwenguni wamekuwa wakiuza hakimiliki ya nyimbo zao kwa kampuni mbali mbali.

Januari mwaka huu Justin Bieber aliuzia kampuni ya Hipgnosis Songs Capital hakimiliki za nyimbo zake kwa dola milioni 200.

Mwaka jana Bob Dylan naye aliuza hakimiliki za nyimbo zake zote kwa kampuni ya Sony.

Website | + posts